Uncharted Knowledge Wisdom From Previous Realities View as JSON for agents & LLMs

Bible & Christianity

Swahili Bible (NT): 2 John

1:1 Mimi Mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule, pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda ninyi, 1:2 kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. 1:3 Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo. 1:4 Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru. 1:5 Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. 1:6 Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri niliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo. 1:7 Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu akawa binadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni Adui wa Kristo. 1:8 Basi, jihadharini ninyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishugulikia, bali mpate tuzo lenu kamili. 1:9 Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana. 1:10 Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. 1:11 Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu. 1:12 Ninayo mengi ya kuwaambieni lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike. 1:13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.